KAMPUNI ya Broadway Group of Companies (Bakex Millers) imetoa mchango wa Sh12.5 milioni na mifuko kiasi cha beli 10,000 za unga ili kusaidia watu walioathirika na njaa kufuatia janga la Covid-19.
Mkurugenzi wa kampuni hizo, Bw Bimal Shah, alisema kufuatia mkurupuko wa homa ya corona, mambo mengi yamegeuka kote ulimwenguni.
“Nchi za Uropa na Asia ndizo zimeathirika kabisa kutokana na janga hilo. Kwa hivyo, sisi hapa Kenya ni sharti tujipange kwa lolote lile,” alisema Bw Shah.
Alisema msaada huo utasambazwa katika kaunti tofauti hapa nchini.
Baadhi ya kaunti zitakazonufaika ni pamoja na Nairobi, Kiambu, Isiolo, Embu, Laikipia, Kirinyaga, Makueni na hata Nakuru.
Hafla hiyo iliyofanyika Jumanne, ilihudhuriwa na Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, Mkurugenzi wa Benki ya Absa Bw Jeremy Awuori, Eddy Njoroge, na George Muhoho ambao wako katika kamati ya Covid- 19 Fund, na mkurugenzi wa Devki Rolling Mills ya Ruiru, Bw Raval Devki.
Nyongeza
Alisema kampuni yake inazidi kuwajali wafanyakazi wake kwa sababu hivi majuzi kila mfanyakazi alipata nyongeza ya mshahara kufuatia jinsi hali ya maisha ilivyo.
Alizidi kueleza kuwa kutokana na ukarimu huo wafanyakazi hao nao walitoa mchango wao wa Sh100,000 ili kusaidia katika mfuko wa Covid-19 Fund.
Alisema kutokana na ukarimu huo wafanyakazi kadha waliajiriwa kazi ya kudumu kutoka kuwa vibarua.
“Kampuni yetu haifanyi ukarimu huo kwa sababu ya kisiasa na kutaka kujionyesha lakini ni kujitolea kwa moyo,” alisema Bw Shah.
Gavana Nyoro alipongeza juhudi zilizotekelezwa na kampuni ya Broadway Company Ltd.
“Sisi kama Kaunti ya Kiambu tumejiandaa vilivyo dhidi ya janga hilo la corona. Tunastahili kuwa tayari kwa lolote lile,” alisema Dkt Nyoro.
Alipongeza juhudi zinazotekelezwa na wahudumu wa afya za kushughulikia wagonjwa tofauti ili kuokoa maisha yao.
Alisema hospitali ya Tigoni imewekwa tayari kuwa ya wagonjwa walioambukizwa Covid-19 na tayari ina vitanda 200.
Alisema tayari masoko mengi yamepulizwa dawa na watu wataendelea na biashara zao.
Mbali na mipango hiyo gavana huyo alisema mipango muhimu wanaoshughulika nayo kwa sasa ni ugavi wa chakula kwa walioathirika katika kaunti mzima ya Kiambu.
Alisema kulingana na makadirio yao wanahitaji tani 960 za unga wa mahindi, halafu mchele, na maharage wanahitaji jumla ya tani 1,200. Nayo sukari ni tani 500.
“Tutahakikisha kila mmoja wa wanaohitaji msaada anapata haki yake bila kubagua ambapo tutatumia machifu na kamati ya watu walioteuliwa kugawa chakula hicho,” alisema Dkt Nyoro.
Mkurugenzi wa benki ya Absa Bw Awuori alisema tayari kamati ya kupokea fedha za Covid-19 Fund imepokea takribani Sh2 bilioni ambazo alisema zitalindwa vyema kuhakikisha zinasaidia wote walioathirika.
Alipongeza kampuni ya Broadway Group of Companies kwa kujitolea kusaidia wasiojiweza.
“Hiyo ni njia moja ya kuonyesha ukarimu,” alisema Bw Awuori.
Bw Devki alitoa mchango wake wa Sh1 milioni zitakazosaidia mfuko wa Covid-19 Fund.
Alitoa mwito kwa wahisani wengine kujitolea ili kufanikisha mwito wa serikali wa kuchangisha fedha hizo za kusaidia kukabili Covid- 19.
Hapo awali pia alitoa Sh100 za kununua hewa za vifaa vya kuwasaidia wagonjwa kupumua – ventilators – ili kutumika katika hospitali tofauti.
Source: https://taifaleo.nation.co.ke/?p=51015